Monday, October 11, 2010
Kenya na Uganda zang'ang'ania medali
Mateelong ashinda dhahabu
Wanariadha wa Kenya walinyakua medali zote tatu, dhahabu, fedha na shaba katika mbio za mita elfu tatu kuruka viunzi.
Richard Mateelong aliongoza msafara wa Wakenya alipomaliza baada ya muda wa dakika 8:16:39 akifuatiwa na Ezekiel Kemboi naye bingwa wa Olimpiki Brimin Kiprop Kipruto alibaki kuikumbatia medali ya shaba.
"Ni matokeo mazuri sana", alisema Mateelong huku akikiri kwamba "kilikuwa kibarua kigumu sana lakini nimefurahi kupata ushindi".
Akizungumza baada ya mashindano, Kipruto alisema nia yao kubwa ilikuwa kuhakikisha kwamba wananyakuwa medali zote tatu.
Kipsiro anyang'anya Wakenya tonge mdomoni
Kipsiro awapiku Wakenya na kunyakua dhahabu ya pili
Baadaye, Nancy Jebet Langat pia kutoka Kenya alishinda medali ya dhahabu katika mbio za mita 800 ikiwa ni taji la pili baada ya kushinda mita 1,500 mnamo mwisho wa wiki.
Pambano la mita 800 lilizua msisimko katika uwanja wa Jawaharlal Nehru wakati mwenyeji Tintu Luka alijitosa mbele kwa mikikimikiki huku akishangiliwa kwa mayowe na vifijo.
Mkenya mwingine Winny Chebet ambaye alionekana kuwania nafasi ya pili, alianguka akiwa amesalia na mita 10 peke yake kumaliza mbio hizo.
Lakini baada ya kuongoza mzunguko wa kwanza Tintu alianza kupwaya, pumzi ikamwishia, wenzake wakampita na akamaliza mnamo nafasi ya sita.
Ilikuwa ni siku ya kufana pia kwa Uganda baada ya Moses Ndiema Kipsiro kushinda medali yake ya pili baada ya kuwapiku wapinzani kutoka Kenya katika mbio za mita elfu 10.
Wiki iliyopita Kipsiro alionyesha ukali wake alipotamba mbele na kushinda dhahabu katika mbio za elfu tano.
Katika mbio za mita elfu 10, nusura Wakenya wangenyakuwa dhahabu lakini Kipsiro alikataa kata kata huku akitwaa ushindi kwa dakika 27:57.39. Mkenya Daniel Salel alisalia na fedha huku Joseph Birech akijishindia shaba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment