Wednesday, November 24, 2010

Mshambuliaji wa Inter Milan Samuel Eto'o amefungiwa kucheza michezo mitatu


Samuel Eto'o

Samuel Eto'o afungiwa michezo mitatu
Mshambuliaji wa Inter Milan Samuel Eto'o amefungiwa kucheza michezo mitatu ya Ligi ya Italia maarufu Serie A, baada ya kumtwanga kichwa mchezaji wa klabu ya Chievo, Bostjan Cesar.

Wachezaji hao wawili walikumbana katika dakika ya 38 ya mchezo ambapo Inter walilazwa mabao Inter 2-1 na Chievo siku ya Jumapili, baada ya Cesar kurusha ngumi hafifu iliyompata Eto'o usoni.

Eto'o, ambaye tayari ameshafunga mabao 17 msimu huu, aliondoka katika eneo alilorushiwa ngumi, lakini baadae akamgeukia mgomvi wake na kumtwanga kichwa kifuani.

Mwamuzi hakuchukua hatua yoyote kutokana na tukio hilo, lakini Shirikisho la Soka la Italia, limemfungia Eto'o baada ya kupitia ushahidi wa mkanda wa video.

Ligi ya Italia ilishawahi kutumia ushahidi wa video siku za nyuma na walimfungia mshambuliaji wa Fiorentina Alberto Gilardino kucheza michezo miwili baada ya kufunga bao kwa mkono.

Taarifa iliyotolewa na Ligi hiyo ya Italia, Serie A, imesema kichwa alichorusha Eto'o's ambacho waamuzi hawakukiona, ni shambulio la aibu na ni utovu wa nidhamu usiokubalika.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Cmeroon, ambaye amepigwa faini ya euro 30,000, ataweza kucheza siku ya Jumatano katika mechi ya Ligi ya Ubingwa wa Ulaya dhidi ya FC Twente.

Lakini kufungiwa kucheza mechi tatu za ligi ya Italia, ni pigo kubwa kwa kocha wake Rafael Benitez, ambaye hivi sasa anakabiliwa na wachezaji wengi majeruhi, akiwemo mpachika mabao hatari Diego Milito.

Mabingwa hao watetezi wa Italia, msimu huu wamebanwa baada ya kupoteza mechi kadha na kwa sasa wanashikilia nafasi ya sita ya msimamo wa ligi, pointi tisa nyuma ya mahasimu wao wakubwa , AC Milan.

Taarifa za vyombo vya habari zimekuwa zikidai huenda kocha Rafael Benitez akafutwa kazi ikiwa Inter Milan ambao ni mabingwa watetezi, watapoteza mechi na FC Twente.

Hata hivyo Rais wa klabu hiyo Massimo Moratti amekanusha madai hayo na kusema ataendelea kumuunga mkono Benitez

No comments:

Post a Comment