Tuesday, July 20, 2010

Mabomu Yaua 64 Wakiangalia Kombe la Dunia Uganda


Watu 64 akiwemo Mmarekani mmoja wamefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa nchini Uganda kutokana na mabomu mawili yaliyolipuka sehemu mbili tofauti ambazo mamia ya watu walijazana kuangalia fainali ya kombe la dunia kati ya Hispania na Uholanzi.
Zaidi ya watu 64 wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti ya milipuko ya mabomu mjini Kampala katika maeneo ambayo mamia ya watu walijazana kuangalia fainali ya kombe la dunia.

Raia mmoja wa Marekani ni miongoni mwa watu waliouawa na mabomu hayo. Hadi sasa polisi wamethibitisha vifo vya watu 23 vilivyotokea katika mgahawa wa Kiethiopia na klabu ya rugby.

Mabomu hayo yalilipuka katika sehemu mbili tofauti yakipishana muda kwa dakika 10.

"Taarifa tulizo nazo zinaonyesha kuwa watu 13 wamefariki katika mgahawa wa Ethiopian Village na wengine wengi wamejeruhiwa vibaya huku watu wengine 10 wamefariki katika klabu ya rugby", alisema inspekta wa polisi, Kale Kayihura.

Polisi wamesema kuwa watu wengi wamejeruhiwa vibaya katika matukio hayo mawili ambayo yalitokea huku mamia ya watu wakiwa wamejazana kuangalia mechi ya fainali ya kombe la dunia kati ya Uholanzi na Hispania ambapo Hispania ilitawazwa mabingwa kwa ushindi wa bao 1-0.

"Mabomu yalilipuka wakati kumbi za baa zikiwa zimefurika watu waliokuwa wakiangalia mechi ya fainali ya kombe la dunia", alisema msemaji wa polisi, Judith Nabakooba.

Kundi la wanamgambo wa Somalia la Al-Shabbab ndilo linalohisiwa kufanya shambulizi hilo kutokana na ahadi waliyoitoa miaka michache iliyopita kuwa watafanya mashambulizi nchini Uganda na Burundi kwakuwa nchi hizo zimepeleka majeshi yake nchini Somalia kuisaidia serikali iliyopo madarakani.

Jumla ya wanajeshi 5000 toka Uganda na Burundi wapo mjini Mogadishu ili kuilinda serikali iliyopo madarakani.

No comments:

Post a Comment