Saturday, July 24, 2010

JAMHURI JAZZ BAND, ONDOA WASIWASI


Sijui wewe mwenzangu,ila mimi nahisi siku zinakwenda kwa kasi ya ajabu.Wiki inavyokatika huwa nashindwa kujua hata imeishaje! Nikizingatia kwamba tayari tupo katika ngwe ya pili ya mwaka 2010,napata wasiwasi kidogo.Je ntatimiza malengo yangu niliyojiwekea siku ile ya mwaka mpya wakati ving’ora vikilia kutoka bandarini,taa zikiwaka na kuzimika?

Pamoja na kupatwa na wasiwasi ninapoangalia mzunguko wa saa,huwa napata faraja kujua kwamba wiki ndio inakatika na kwa maana hiyo,weekend imewadia.Ni muda wa kupumzisha akili kidogo.Ni muda wa kuburudika na “Zilipendwa” kama ilivyo jadi yetu hapa BC. Najua pengine bado unawajibika wakati wa weekend.Sawa.Lakini kuna pumziko fulani.Barabarani magari yanakuwa yamepungua.Mitaani kunakuwa kweupe kidogo.

Kwa upande mwingine,fainali za Kombe la Dunia la FIFA ndio zishamalizika.Pweza Paulo kajipatia umaarufu wa kutosha.How could he be right all the time? Naambiwa sio Paulo Pweza peke yake aliyekuwa sahihi katika utabiri.Nasikia hata Spika wa Bunge letu,Mheshimiwa Sitta alitabiri kwamba Spain “itafanya vizuri sana”. Lakini kali ni kutoka kwa Nabii Joshua(kama hujawahi kumsikia nisamehe).Yeye alitabiri vyema kabisa mechi ya ufunguzi katika ya South Africa na Mexico. Alisema Mungu kamwambia South Africa watafunga goli kwanza ila wasipolilinda litarudishwa!.Upo hapo? Mambo ya common sense hayo.

Enewei,fainali zimeisha vyema.Afrika Kusini wametutoa kimasomaso maana jamaa wa magharibi walikuwa wamechachamaa kweli wakisema Afrika hakuna nchi inayoweza kuandaa mashindano makubwa kama yale. Kumbe hawakujua kwamba waafrika,pamoja na mambo yetu yote,tunasikilizana.Wale “chinjachinja” wakaambiwa tulizeni mzuka wakati wa fainali na kweli jamaa wakatulia kimyaa.Ngoma ipo kwa Brazil sasa.Jamaa wanaanda fainali za mwaka 2014.Kule napo nasikia fujo kama kawaida.Kuna Favela.

Turudi kwenye burudani sasa.Leo tunao Jamhuri Jazz Band.Wimbo unaitwa Wasiwasi Ondoa. Jamhuri Jazz Band ilianzishwa katika miaka ya 50s kule mkoani Tanga.Wakati huo kulikuwa hakuna Tanzania bali Tanganyika.Mwanzoni bendi hiyo iliitwa Young Nyamwezi Band.Mabadiliko yalifuata baada ya kupata ufadhili wa bwana mmoja aliyeitwa Joseph Bagabuje.Baadaye Bagabuje alikuja kuwa mtanganyika wa kwanza kuwa Meneja wa Amani Tea Estate.

Miongoni mwa wanamuziki ambao baadaye walijiunga na bendi hiyo na kuisaidia kukua zaidi ni pamoja na wana-ndugu Wilson Kinyonga na George Kinyonga. Walijiunga na Jamhuri Jazz Band mwaka 1966 kabla hawajimega mwaka 1970 na kwenda kuunda Arusha Jazz Band na baadaye Simba Wanyika.

No comments:

Post a Comment