Saturday, July 24, 2010

MBAYA WANGU YUKO WAPI?


Kama ipo wiki ambayo nilitamani sana ifikie ukingoni,hii bila shaka ni mojawapo.Kwa kiasi fulani nilikuwa nimeshachoka na “watangaza nia”.Naona kila mtu anaitumia ipasavyo haki yake ya msingi.Watetezi wanasema huo ndio ukuaji wa demokrasia.


Wasiwasi wangu ni kwamba kwa namna fulani,imeshageuka kuwa fasheni.Si unajua tunavyopenda kuigana?Mmoja akianza kitu basi wengine ni lazima wafuate.Unataka kuniambia umesahau biashara ya salon ilipoanza? Au daladala za watu binafsi ziliporuhusiwa?


Kwa “waliotangaza nia” na kuchukua fomu, naomba uwasikilize kwa makini.Sentensi na misemo inakuwa ni ile ile.Ahadi zinakuwa zinafanana.Huyu akiahidi kwamba ataanzisha kituo cha televisheni mahali ambapo hata umeme haujafika,mwingine bila hata kufikiria naye anasema hivyo hivyo.Mwananchi wa kawaida,kichwa kinapata kizunguzungu.Amwamini nani?Mbona wote wanaongea sawa na ahadi zao zinafanana? Labda nikamsikilize kasisi kanisani au sheikh msikitini? Mmh huko nako kuna mengi.Kama jiwe la msingi liliwekwa na fulani,kuna jipya?


Kwa hiyo nikawa natamani wikiendi iwadie kwani sijasikia sana kuhusu wanaotangaza nia katika siku za wikiendi.At least sio hadharani.Labda kule kwenye moja moto,moja baridi.Kichwa kikianza kuwa kizito,lugha inabadilika na sera za kweli zinaanza kutolewa.Ngoja wanichague,I can’t wait kuwa na “shangingi” langu na dereva.Mimi na safari,safari na mimi.Pembeni toto ya kona.Mheshimiwa Mbunge(MP).


Enewei,maisha yanasonga.Burudani ni jadi yetu hapa.Wimbo wa leo unaitwa Namsaka Mbaya Wangu
kutoka kwao Dar-es-salaam Jazz Band chini ya Jabali la Muziki,Hayati Marijani Rajabu.


Dar-es-salaam Jazz Band ni mojawapo ya bendi za kwanza kwanza kubwa nchini Tanzania.Ni bendi ambayo wanamuziki wengi sana wakongwe walipitia.Kwa mfano kina Ahmed Kipande, Patrick Balisidya, Juma Mrisho, Dancan Njilima, Moshi William (Tx), Juma Akida, Emmanuel Joseph, Hamis Nguru na wengine wengi.Iliundwa kufuatia mmeguko kutoka bendi iliyokuwa inajulikana kama African Association Jazz Band iliyokuwa na makao yake makuu,Kariakoo katika miaka ya 30s. Katika miaka ya 30s mpaka 40s bendi kubwa zilibakia kuwa African Association Jazz Band na Dar-es-salaam Jazz Band.


Baada ya kumalizika kwa Vita Kuu ya Dunia ya Pili,huku veterans wakirejea huku wakiwa na santuri mbalimbali kutoka ughaibuni,picha ya starehe za mjini nazo zikaanza kubadilika kidogo.Meneja wa Dar Jazz Band wakati huo alikuwa jamaa aliyeitwa Athumani Muba(Mzee Muba) ambaye alikuwa ni miongoni mwa waanzilishi wa bendi hiyo pamoja na kina Hamisi Machapati.In fact nyumba yake pale mitaa ya Kariakoo-Gerezani ndio ilikuwa “clubhouse”.


Baadaye katika miaka ya 60s bendi hiyo ilikuwa chini ya uongozi wake Michael Enoch,mpiga gitaa la solo maarufu ambaye inasemekana ndiye Mwalimu wa wanamuziki wengi sana nchini Tanzania.Baadaye Enoch alikuja kuwa mpiga saxophone mzuri na ambaye saxophone yake inasikika katika nyimbo nyingi zilizotamba za Mlimani Park Orchestra(Sikinde) alikohamia baadaye.


Lakini kwa wengine wengi,Dar Jazz Band inayokumbukwa ni iliyokuwa chini ya Jabali la Muziki,Marijani Rajab(RIP)

No comments:

Post a Comment