Friday, July 23, 2010

Jol kuifunza Fulham


Martin Jol anatazamiwa kutajwa kuwa meneja mpya wa Fulham.

Kwa mujibu wa idara ya michezo ya BBC, kocha huyo wa Ajax amekuwa na mazungumzo ya awali na klabu hiyo ya London, na kuwa atazungumza na maafisa wa Fulham baadaye wiki hii kuzungumzia mkataba wake.


Martin Jol kurejea tena London

Jol, mwenye umri wa miaka 54 aliwahi kuifundisha klabu nyingine ya London ya Tottenham kati ya mwaka 2004 na 2007. Anatazamiwa kuchukua nafasi ya Roy Hodgson aliyejiunga na Liverpool tarehe mosi mwezi Julai.

Kocha wa Ivory Coast, Sven Goran Ericksson alikuwa pia akitajwa kuchukua nafasi hiyo ya Fulham. Hakutakuwa na taarifa rasmi kuhusu kuteuliwa kwa Jol, kabla ya Fulham kwenda Sweden kwa ajili ya michezo ya kabla ya msimu kuanza, lakini Jol anatarajiwa kuungana na kikosi hicho baadaye.

Kocha wa timu ya taifa ya Marekani Bob Bradley na kocha wa Uswisi Ottmar Hitzfield pia walikuwa wakitajwa, lakini Hitzfield alijitoa, huku taarifa ya chama cha soka cha Marekani ikisema itaongeza mkataba wa kocha wake wa taifa.

Jol aliyefukuzwa kazi na Tottenham mwezi Oktoba mwaka 2007, bado anamiliki nyumba nchini England na taarifa zinasema raia huyo wa Uholanzi atapewa mkataba wa kuendelea. Ingawa Fulham ilicheza fainali ya ligi ya Europa mwezi may mwaka huu, Ajax itakuwa ikicheza ligi ya mabingwa wa Ulaya mwezi Septemba, iwapo itaweza kufuzu.

No comments:

Post a Comment