Saturday, July 24, 2010

Rashid Matumla au ukipenda “Snake Boy”, juzi ilikuwa ndio mwisho wake


Kila jambo lina mwisho wake. Kwa Bondia mkongwe na mahiri nchini Tanzania,Rashid Matumla au ukipenda “Snake Boy”, juzi ilikuwa ndio mwisho wake katika mchezo wa ndondi akiwa kama mchezaji.


Baada ya pambano lake na Bondia mwingine anayekuja juu katika mchezo huo,Mada Maugo,lililofanyikia katika Ukumbi wa PTA uliopo kwenye uwanja wa maonyesho wa Mwalimu Nyerere Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam, Matumla alitangaza kustaafu rasmi au kutundika “gloves” kama wenyewe wanavyosema.Katika pambano hilo,Matumla alipoteza kwa jumla ya pointi 98-95.Pambano hilo ambalo halikuwa la kuwania ubingwa wowote,lilikuwa la raundi kumi.


Matumla ambaye aliyewahi kufanya makubwa katika medani ya ngumi za kulipwa, alifikia hatua hiyo baada ya miaka kadhaa kushauriwa na wadau kadhaa akiwamo baba yake mzazi kuachana na mchezo huo kutokana na umri kumtupa mkono, bila mafanikio.


Rashid Matumla alizaliwa tarehe 16/5/1968 mkoani Tanga. Mpaka anastaafu na tangu aanze kupigana ngumi za kulipwa,ameshinda mapambano 40(kati ya hayo 30 kwa Knock Out) na ameshindwa katika mapambano 14(manne kati ya hayo alipigwa kwa KnockOut) na ametoka draw katika mapambano 2. Kwa ujumla amepambana katika raundi 373. Mpaka anastaafu katika ulimwengu wa ndondi za kulipwa katika uzito wa kati(Middle Weight),Matumla anashikilia nafasi ya 299 kati ya wanandondi 1107 wanaotambulika na walio active katika uzito huo.Kwa nchini Tanzania,amestaafu akiwa katika nafasi ya 5 miongoni mwa mabondia 29 wanaotambulika na ambao bado wapo active.Walio mbele yake ni Karama Nyilawila,Thomas Mashali,Mada Maugo, na Francis Cheka ambaye ndiye nambari 1 kwa hivi sasa nchini Tanzania.


Baada ya kustaafu Matumla amesema ushiriki wake katika mchezo huo namba mbili kwa kuwa na wapenzi wengi duniani nyuma ya soka,utakuwa katika nafasi ya ukocha.Amesema hivi sasa atajikita katika kuibua vipaji vya ndondi miongoni mwa vijana.


Tunamtakia Rashid Matumla au “Snake Boy” maisha mema katika kustaafu.

No comments:

Post a Comment