Tuesday, July 27, 2010

Uso wa kupachikwa waonekana


Oscar na mmoja wa madaktari wake


Mhispania mmoja aliyepachikwa viungo vya uso mzima wa mtu mwengine uliofanyika kwa mara ya kwanza duniani ameonyesha uso wake ulivyo kwa sasa hadharani mbele ya televisheni.

Mtu huyo mwenye umri wa miaka 31 ameishukuru familia iliyomfadhili kwa kutoa viungo hivyo na wataalamu waliompa uso mpya mwezi Machi katika hospitali ya chuo cha Vall d'Hebron, Barcelona.

Kupigwa risasi kwa bahati mbaya kwa mtu huyo kulimaanisha kuwa ngozi yake ya uso na misuli-ikiwemo ya poa na midomo- kulitakiwa kubadilishwa upya.

Madaktari wamesema Mhispania huyo anaweza kutarajia hisia zake za uso kurejea kwa asilimia 90.

Baada ya kupata ajali miaka mitano iliyopita mtu huyo alikosa uwezo wa kupumua, kumeza au hata kuzungumza vizuri.

Sasa mtu huyo, anayetambulika tu kama Oscar, bado anahangaika kuzungumza kwa umakini na atahitaji miezi kadhaa ya kufanyiwa matibabu ya mwili.

Alisema katika mkutano na waandishi wa habari: " Marafiki zangu, nataka kuwashukuru wasimamizi wa hospitali, wote walionipa matibabu, familia iliyonifadhili na zaidi ya wote familia yangu inayonisaidia siku hizi."

Iliamuliwa uso wa Oscar ubadilishwe upya baada ya upasuaji huo kufanyika mara tisa bila mafanikio.

Kundi la wataalamu 30 lilifanya upasuaji huo uliodumu kwa saa 24 tarehe 20 Machi huko Barcelona.

Ukiongozwa na Dr JP Barret, timu hiyo imerekebisha misuli, pua, midomo, taya, paa la kinywa, meno yote, kitefute (cheek bones), na utaya kwa njia ya upasuaji.

Ni upasuaji wa mwanzo wa uso mzima kufanyika duniani, kwani nyengine 10 zilizofanyika hapo awali zilikuwa sehemu tu ya uso.

Mafanikio ya mwanzo ya upachikaji wa viungo vya uso kwa mtu mwengine ulifanyika nchini Ufaransa mwaka 2005 kwa Isabelle Dinoire, mwanamke wa umri wa miaka 38 ambaye aliumizwa vibaya na mbwa wake.

No comments:

Post a Comment