Tuesday, July 20, 2010

Warwanda 'wana uhuru wa kuchagua"

Rais wa Rwanda Paul Kagame ameahidi uchaguzi wa mwezi ujao utakuwa huru, akipinga ukosoaji wa hivi karibuni uliotolewa na mashirika ya kutetea haki za binadamu.

Akizindua kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa Agosti 9, " Wapiga kura wa Rwanda wana uhuru wa kuchagua."

Wakosoaji kadhaa wameuliwa au kushambuliwa hivi karibuni, afisa mmoja mwandamizi alikuwa akizikwa huku Bw Kagame akiwa anazungumza.
Serikali imekana kuhusika na mauaji yeyote.

Mwandishi wa BBC Geoffrey Mutagoma mjini Kigali amesema maelfu ya wafuasi wa Bw Kagame- wengi wakiwa wamevaa rangi za chama ikiwa ni nyekund, nyeupe na bluu- wamejaza uwanja wa taifa wa Amahoro na wengi wameshindwa kuingia.

Vyama vingine vitatu vimezindua kampeni zao lakini vyote vinaonekana kuwa karibu na Rais- viwili vimekuwa serikalini tangu mwaka 1994.

Vyama vingine vingi vya kisiasa vimezuiwa kushiriki katika uchaguzi.

' Si mjinga'
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kampeni hizo, Bw Kagame alisema anahisi chama chake kitarudi madarakani: " Nina imani kuwa raia wa Rwanda watachagua kushirikiana na RPF."

Saa chache kabla ya kampeni kuanza, makamu wa Rais wa chama cha Democratic Green, Andre Kagwa Rwisereka alizikwa.

Mwili wake ambao karibu wote ulikuwa umekatwa ulikutwa Butare kusini mwa Rwanda wiki iliyopita baada ya kuripotiwa kutojulikana alipo.

Chama chake hakiwezi kushiriki kwenye uchaguzi, na kinadai serikali imekataa kukisajili.

Kumekuwa na matukio mengine yaliyozua wasiwasi katika miezi ya hivi karibuni, ikiwemo kifo cha mwandishi maarufu wa habari, jaribio la kumwuua aliyekuwa mkuu wa majeshi, na wengi kukamatwa huku kukiwa na ripoti za kugawanyika katika jeshi la Rwanda.

Serikali imekana kuwavuruga upinzani.

Waziri wa mambo ya nje Louise Mushikiwabo ameliambia shirika la habari la AP, " Najua wengi hawatotuona kama ni serikali ya kuigwa, lakini si wajinga, na hatutajaribu kuua watu watatu kwa mpigo kabla ya uchaguzi- uchaguzi ambao tunaamini kuwa Rais Paul Kagame atashinda."

Lakini mwandishi wetu alisema si kila mmoja anaamini kauli hiyo.

No comments:

Post a Comment