Thursday, August 12, 2010
FIFA yaichunguza Korea Kaskazini
Shirikisho la mchezo wa soka duniani FIFA limeanzisha uchunguzi kufuatia madai kuwa utawala wa Korea Kaskazini unawanyanyasa wachezaji wake wa timu ya taifa, kufuatia matokeo mabaya katika michuano ya Kombe la Dunia iliyokamilika nchini Afrika Kusini.
Katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Brazil kikosi hicho kilicheza mchezo bora hatua ambayo ilichochea, runinga ya taifa kuonyesha mechi yao iliyofuatia, kitendo ambacho hakijawahi kufanyika katika historia ya nchi hiyo.
Wachezaji wa Korea Kaskazini
Lakini Korea ilipoteza mechi hiyo baada ya kunyukwa mabao saba kwa bila na Ureno.
Matokeo hayo yalichukuliwa kuwa yameiletea aibu kubwa nchi ya Korea ya Kaskazini.
Madai kwamba kocha wa timu hiyo Kim Jong Hun amehukumiwa kifungo cha kazi ngumu katika ujenzi wa nyumba hayakuweza kuthibitishwa.
Inaelekea hivi sasa FIFA imechochewa na taarifa zaidi kutoka chama cha kandanda cha Korea ya Kusini na imetuma barua kwa Korea ya Kaskazini kama madai hayo ni kweli.
Na pia inachunguza kama kuna ukweli wowote kwa madai kwamba wachezaji wa Korea ya kaskazini walikabiliwa na vikao vya muda wa saa sita kuwapiga msasa kiidiolojia mbele ya watu 400 katikati ya jiji la Pyongyang.
Madai hayo yalijitokeza kwanza katika ripoti ya kituo kimoja cha redio kutokana na mahojiano na mfanyabiashara mmoja wa Kichina ambae inasemekana alikuwa na fungamano na maafisa wa Korea ya Kaskazini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment