
Ni baada ya siku chache tu kwa msaada wake Allah Karim utakuwa unapumua na kuishi ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Mwezi ambao huwapa waislamu fursa ya kuitekeleza mojawapo ya nguzo tano za Uislamu, swaumu ya Ramadhani. Katika kuuheshimu, kuutukuza na kuuenzi mwezi huu mtukufu, Mtumishi wa uma {WEBSITE UISLAMU}, itakutumikia kwa kukuletea mfululizo wa makala maalumu zihusianazo na mwezi wako huu. Lengo kuu la makala hizi likiwa ni kukumbusha wewe msomaji wetu:-
Utukufu wa mwezi wa Ramadhani ili uuthamini, kwani asiyekujua hakuthamini.

Haya ndiyo malengo mama ya makala hizi ambazo tunatumai kwa msaada na taufiq yake Allah yatakunufaisha na kujibu maswali yako mengi. Ambayo kwa namna moja au nyingine yamekuwa yanakutatiza kuhusiana na swaumu hii ya Ramadhani.
Naam, Ramadhani hiyo mlangoni mwako inabisha hodi. Wewe kama muislamu umejiandaje kuupokea mwezi wako huu mtukufu? Je, wewe ni mmoja wa wale wanaoupokea mwezi wa Ramadhani kwa kile kinachojulikana kama VUNJA JUNGU?







Elewa kwa mtindo na mtaji wako huo siku ya kiyama Allah atakuambia ujilipe wewe mwenyewe kwa kuwa yeye hakukuamrisha kufanya ibada kwa utaratibu huu unaokwenda nao sasa.
Ndugu mpenzi hebu ihurumie nafsi yako kwa kuitegea sikio la usikivu kauli hii tukufu ya Mola wako: “ANAYEFANYA MEMA ANAJIFANYIA (mwenyewe) NAFSI YAKE, NA MWENYE KUTENDA UBAYA NI JUU (ya nafsi) YAKE (vile vile)…” [41:46]
Aya inakuongoza kutambua kwamba unapovunja jungu, hufanyi hivyo ila ni kwa hilaki na maangamivu ya nafsi yako wewe mwenyewe leo hapa duniani na kesho kule akhera. Ambapo utapewa daftari la amali zako uikute na vunja jungu yako, hapo ndipo utasema: “…OLE WETU! NAMNA GANI MADAFTARI HAYA! HAYALIACHI DOGO WALA KUBWA ILA YAMELIDHIBITI (yameliandika)! NA WATAKUTA YOTE YALE WALIYOYAFANYA YAMEHUDHURIA HAPO; NA MOLA WAKO HAMDHULUMU YO YOTE”. [18:49]

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Jibril alinijia na akaniambia: Ewe Muhammad! Ishi utakavyoishi, hakika wewe ni mwenye kufa. Na penda ukipendacho hakika utatengana nacho, na tenda ulitakalo hakika utalipwa kwalo…” Al-Baihaqiy
Elewa ewe ndugu mpenzi ukiwa mwana kuelewa, elewa kwamba kwa mujibu wa hadithi hii:-
Vunja jungu yako ina mwisho wake ambao ni kufa kunakoashiria mwanzo wa safari ngumu ya kuhudhurishwa mbele ya Mola wako. Hii ndiyo siku anayoitaja Mola wako kwa kauli yake tukufu: “NA IOGOPENI SIKU AMBAYO MTARUDISHWA KWA ALLAH, KISHA VIUMBE WOTE WATALIPWA KWA UKAMILIFU YOTE WALIYOYACHUMA; NAO HAWATADHULUMIWA”. [2:281]
Lewa sana kwani pesa ni zako,zini sana na endelea kuvunja jungu, lakini tambua kuwa iko siku moja utalipwa kwa yote uliyoyatenda hapa duniani: “BASI ANAYEFANYA WEMA (hata) WA KIASI CHA UZITO WA MDUDU CHUNGU ATAONA JAZAA YAKE. NA ANAYEFANYA UOVU (hata) WA KIASI CHA UZITO WA MDUDU CHUNGU ATAONA JAZAA YAKE”. [99:7-8]

Ewe mvunja jungu wee! Hebu waidhika na sehemu hii ya kauli ya swahaba wa Mtume;Sayyidna Abdullah Ibn Abbas-Allah amuwiye radhi:
“Ewe mtenda dhambi wee! Usijiaminishe na matokeo ya dhambi yako na tambua kwamba kiifuatiacho dhambi hiyo ni kikubwa kuliko dhambi yenyewe.
Kwani kule kutokuwaonea kwako haya malaika walioko kuliani na kushotoni kwako wakati unapofanya dhambi, hakupungui kuwa ni dhambi.
Na kicheko chako wakati unatenda dhambi na ilhali hujui Allah atakufanya nini, ni kikubwa zaidi kuliko hiyo dhambi uitendayo.
Na kuichelea kwako dhambi unapofanikiwa kuitenda, ni kukubwa zaidi kuliko hiyo dhambi yenyewe.
Na kuihuzunikia kwako dhambi kwa kushindwa kuitenda, ni kukubwa zaidi kuliko dhambi husika.
Haya mpenzi mvunja jungu, ikiwa mpaka hapa bado hujawaaidhika na ukaacha kulivunja hilo jungu, hebu zidi kutega sikio:
Mtu mmoja alimwambia Sufyaan Thauriy-Allah amuwiye radhi-nipe nasaha ambazo nikizifanyia kazi sitathubutu kumuasi Allah. Sufyaan akamwambia: Yakumbuke mambo matano:
Je, inastahiki kwako kumuasi Allah na ilhali yeye ndiye anayekuruzuku?
Je, unadhani kuwa wewe unamuasi Allah na ilhali yeye anakuona?
Je, unaweza kumuasi Allah nje ya ufalme/milki yake?
Je, unaweza kuyaakhirisha mauti yakikujia?
Je, siku ya kiyama utakuwa una uwezo wa kujiondoshea adhabu?
Yule mtu akajibu: Siwezi lo lote katika hayo. Sufyaan akamwambia: Basi vipi unathubutu kumuasi yule anayekuruzuku, anakuona, nawe uko katika milki yake, akakuandikia mauti na wala huwezi kuizuia adhabu yake isikufike? Akasema mtu yule: Wallah sitamuasi muda wa uhai wangu.
Hebu nawe mvunja jungu, jiulize maswali matano hayo halafu ndio uamue ama kulivunja jungu au kutokulivunja. Kumbuka ewe ndugu muislamu kwamba:-
Kuvunja jungu ni kumuasi Allah na Mtume wake: “NA ANAYEMUASI ALLAH NA MTUME WAKE, NA KUIRUKA MIPAKA YAKE (Allah) ATAMUINGIZA MOTONI. HUMO ATAKAA MILELE NA ATAPATA ADHABU ZIFEDHEHESHAZO”. [4:14]
Kuvunja jungu ni kuudhihaki mwezi mtukufu wa Ramadhani. Na kuudhihaki mwezi huu hakumaanishi kingine zaidi ya kuidhihaki Qur-ani Tukufu. Nako huku kuidhihaki Qur-ani, hakika si vinginevyo ila ni kumdhihaki aliyeshushiwa Qur-ani Mtume. Na hakuna anayethubutu kupinga kwamba kumdhihaki Bwana Mtume ni kumdhihaki Allah akiyemtuma. Na huko kumdhihaki Allah ni ukafiri tu na si vinginevyo: “AMA WALE WALIOKUFURU, NITAWAADHIBU ADHABU KALI KATIKA DUNIA NA AKHERA, WALA HAWATAPATA WASAIDIZI WA KUWASAIDIA”. [3:56]
Vunja jungu ni khadaa na ghururi za dunia. Uovu basi si huko kukhadaika, bali ni kushikilia kukhadaika baada ya kutanabahishwa.
No comments:
Post a Comment