Thursday, August 12, 2010

Gavana akutana na Twiga


Timu ya soka ya wanawake, Twiga Stars ya Tanzania, siku ya Jumanne iliweza kuyatembelea makao makuu ya serikali ya jimbo la Washington, maarufu kama State Capitol.
Bi Christine Gregoire

Gavana wa jimbo la Washington na wachezaji wa Taifa Stars

Wachezaji hao, ambao tangu tarehe 2 Agosti wamekuwa wakifanya mazoezi huko Washington, walikutana na gavana wa jimbo, Bi Christine Gregoire.
Twiga Stars imekuwa ikijinoa kwa mashindano ya wanawake ya bara Afrika, kufanyika nchini Afrika Kusini, mwezi Oktoba.

Timu mbili zitakazofanya vyema zaidi katika mashindano hayo zitaelekea nchini Ujerumani, kushiriki katika mashindano ya wanawake ya Kombe la Dunia nchini Ujerumani.

Twiga Stars imekuwa ikionyesha ari ya kufika Ujerumani, kutokana na mechi za kirafiki nchini Marekani.

Kati ya mfululizo wa ushindi, timu hiyo iliwabwagiza magoli 4-0 timu ya Dos FC jana usiku.

Asha "Mwalala" Rashid alifunga magoli 2, huku Mwanahamis Omary na Fatuma "Kitunini" Mustapha, kila mmoja akiandikisha bao moja.

Mdhamini wa ziara hiyo ya Twiga Stars, Bi Rahma Al-Kharoosi, rais wa kampuni ya mafuta ya RBP Oil and Industrial Technologies, alisema anajivunia kuona kwamba timu hiyo imekuwa ikipata ufanisi, na inapata uzoefu inayohitaji katika kupambana katika mashindano ya Afrika.

Wachezaji wa Twiga Stars walipata nafasi pia ya kumuelezea gavana wa Marekani utaratibu wa kuwachagua wajumbe wa bunge nchini Tanzania.
Wachezaji wa Twiga Stars

Wachezaji wa Twiga na sanamu ya George Washington

Waliwaimbia wenyeji wao wimbo wa Kiswahili, na vile vile kupata fursa ya kuzungumza na gavana.

Gavana aliwatakia kila la heri katika mashindano ya Afrika Kusini, akielezea kwamba hata binti zake wawili ni wachezaji soka.

Ili kupata bahati, wengi wana itikadi ya kuamini ukiisugua pua ya sanamu ya rais wa kwanza wa Marekani, George Washington, nje ya jengo la bunge katika jimbo la Washington, mambo yako huenda yakafanikiwa.

Wachezaji wote wa Twiga Stars waliisugua pua ya sanamu, na kujiongezea matumaini ya kufika katika fainali za Ujerumani, mwaka 2011.

No comments:

Post a Comment